• 9849-xxx-xxx
  • taarifa@elimuraia.com

Muswada wa Tume ya Uchaguzi 2023: Hatua kuelekea Uhuru Wake Kamili au Mwendelezo wa Uhuru wa Mchongo?

Muhtasari

Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi 2023, unaoibua mabishano nchini Tanzania hivi sasa, unaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa muundo na uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambacho ni chombo muhimu katika kuwezesha uchaguzi huru na wa haki. Wakati mvutano ukiongezeka, CHADEMA, chama kikuu cha upinzani, kimetangaza maandamano ya amani ambayo yamepangwa kufanyika Januari 24, 2024, jijini Dar-es-Salaam. Pamoja na mengineyo, lengo la maandamano hayo ni kupinga Muswada tajwa hapo juu wenye kuonekana kupendekeza mabadiliko ya mapambio ambayo hayana tija katika kuimarisha uhuru wa NEC.1 

Kama ilivyo mazoea ya utoaji wa matamko ya kiimla, serikali imetangaza Januari 23 – 24, 2024, kuwa ni “siku ya usafi” jijini Dar-es-Salaam. Na zoezi hilo litasimamiwa na vikosi vya usalama.2 Tamko hili la kuzuia maandamano kwa mgongo wa “siku ya usafi” linaenda kinyume na Kifungu cha 20 (1) cha Katiba ya Tanzania (1977) inayotoa haki kwa wananchi kufanya maandamano ya amani. Pamoja na vikwazo vilivyopo, muda si mrefu tutafahamu ikiwa maandamano haya muhimu yatafanyika kama yanavyopaswa kufanyika. Makala hii inaangazia Muswada wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi 2023 na dhana ya uhuru wa tume ya uchaguzi.

Uhuru wa Tume ya Uchaguzi ni nini?

Uhuru wa tume ya uchaguzi ni msingi wa jamii za kidemokrasia, unaohakikisha usawa, uwazi na uadilifu wa michakato ya uchaguzi. Unahusu uwezo wa tume kufanya kazi kwa uhuru bila kushawishiwa au kuingiliwa na mamlaka nyingine, hasa taasisi za kisiasa au vyombo vya serikali ambavyo vinaweza kuathiri uwezo wake wakutoegemea upande wowote. Uhuru huu kwa kawaida hutolewa katika katiba ya nchi au sheria za uchaguzi, zinazothibitisha kwamba tume kufanya maamuzi kwa uhuru kuhusu mambo muhimu ya uchaguzi, kama vile usajili wa wapigakura, usimamizi wa upigaji kura na utangazaji wa matokeo. Hata hivyo, kiwango cha uhuru kinaweza kutofautiana kulingana na mifumo tofauti ya sheria na miktadha ya kisiasa.

Utafiti wa Uhuru wa Tume ya Uchaguzi

Katika kutathmini uhuru wa tume ya uchaguzi, Cheeseman & Elkrit (2020) wanapendekeza mambo 3 ya msingi ya kuzingatia: Uhuru wa kitaasisi, Kiuongozi na Kifedha.3

Uhuru wa Kitaasisi: Eneo hili hutoa ulinzi wa kisheria ambao hulinda chombo cha uchaguzi dhidi ya kuingiliwa kusikostahili. Pia inajumuisha uhuru wa tume katika michakato ya kufanya maamuzi, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kuamua taratibu zake, kanuni na uendeshaji wa uchaguzi.

Uhuru wa Kiuongozi: Ili kudumisha uwezo wa kutopendelea upande wowote, viongozi na wajumbe wa tume lazima wachaguliwe kwa njia ya uwazi na yenye kuzingatia sifa. Wawe na ulinzi wa ajira zao ili kuzuia kufukuzwa kazi kiholela, jambo ambalo linaweza kudhoofisha uhuru wao katika kutekeleza majukumu yao.

Uhuru wa Kifedha: Tume inapaswa kuwa na bajeti yake iliyotengwa na serikali na kuidhinishwa na Bunge. Iwe na ufadhili wa kutosha na unaojitegemea huhakikisha kuwa haina deni wala haihitaji kulipa fadhila kwa taasisi nyingine yoyote. Fedha hizo zitolewe kwa wakati na moja kwa moja kwa tume. Pia, watendaji wa tume wawe huru kutumia rasilimali zake kwa kadri watakavyoona inafaa.

Hivyo basi, kudai kuwa tume ya uchaguzi ni huru kwa maandishi tu ya kwenye katiba haitoshi. Mifumo ya kisheria inayoimarisha uhuru wa tume husika kitaasisi, kiuongozi, na kifedha lazima iwepo ili kuhakikisha uhuru wa kiutendaji. Hatua hizi ni muhimu ili kudumisha sifa yake ya kutopendelea upande wowote na kuhakikisha inafanya kazi bila kuingiliwa au kushinikizwa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC)

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), Kifungu cha 74, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inapaswa kuwa huru. Hili limefafanuliwa wazi katika vifungu vidogo vya (6) na (7), ambapo inaelezwa kuwa NEC ina jukumu la kusimamia na kuratibu uchaguzi bila kulazimika kutii amri au maelekezo kutoka kwa mtu yeyote, idara ya serikali au chama cha siasa. Aidha, NEC inaelezwa kuwa ni idara inayojitegemea, ikisisitizwa uhuru wake kutoka kwa taasisi nyingine za kiserikali. Hata hivyo, ni muhimu kukiri kwamba wakati katiba inadai kuwa NEC ni huru, utekelezaji wa majukumu yake kwa uhuru unahusisha mambo 3 (matatu), yaani uhuru wa kiuongozi, kifedha na kiutendaji. Masuala haya, kama yalivyoanishwa na Cheeseman & Elkrit (2020), yanahitaji sheria ya kuyaanzisha na kuyasimamia. Ili NEC iweze kutekeleza majukumu yake kwa uhuru wa kweli, ni muhimu kuwepo na mchanganyiko wa masuala hayo matatu.

Masuala ya Kikatiba na Kisheria Yanayoathiri Uhuru wa NEC

Muundo wa NEC unaibua mashaka kuhusu uhuru wake wa kweli kiutendaji. Kwa mujibu wa kifungu cha 74 (1) cha Katiba ya Tanzania (1977), wajumbe wa NEC wanateuliwa na Rais jambo ambalo linaweza kuathiri uwezo wao ya kutopendelea upande wowote na kuwafanya washawishike kisiasa. Pia, Kifungu kidogo cha (10) cha Katiba kinaruhusu wawakilishi kupewa jukumu la kusimamia uchaguzi chini ya uongozi wa NEC4, na hivyo kuzua maswali kuhusu uhuru wao pia.

Aidha, Kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinataja kuwa wakurugenzi wa majiji, manispaa, miji na wilaya watakuwa wasimamizi wa uchaguzi (kama wawakilishi wa NEC) wakati wa uchaguzi, kwa mujibu wa Kifungu cha 74 (10) cha Katiba ya Tanzania (1977).5 Kifungu hiki kimekuwa chanzo cha mzozo mkubwa ndani ya ulingo wa siasa za Tanzania.6 Hii ni kwa sababu inaleta wasiwasi kuhusu uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa kuwa watu hao ni viongozi wa serikali walioteuliwa na Rais ambao wanaweza kuwa na maslahi au upendeleo unaoweza kuathiri utendaji wao wakati wa mchakato wa uchaguzi.

Moja ya majukumu muhimu ya NEC ni kuratibu na kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kuajiri na kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi. Hivyo basi, kuteua maafisa wa serikali kama wasimamizi wa uchaguzi kunazua mgongano wa kimaslahi unaoweza kutokea. Watu hawa wanaweza kuhisi shinikizo la kupendelea chama tawala au Rais aliyewateua. Historia ya chaguzi zilizopita nchini Tanzania imeonyesha kuwepo na upendeleo katika utekelezaji wa majukumu ya NEC. Hili lilidhihirika zaidi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.7

Mapendekezo ya Marekebisho ya NEC

Mambo 3 yaliyopendekezwa na Cheeseman & Elkrit (2020) ni muhimu katika kutathmini uhuru wa tume ya uchaguzi. Ili nadharia ya uhuru wa NEC iweze kuboreshwa kwa vitendo, lazima kuwe na mabadiliko makubwa ambayo yanaimarisha uhuru wake wa kitaasisi, kiuongozi, na kifedha. Ingawa Kifungu cha 9 (1) cha Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi 2023 kinachojumuisha kamati maalum ya usaili kinaweza kugatua mchakato wa uteuzi, ushawishi wa rais katika mchakato mzima wa uteuzi bado ni mkubwa. Kamati ya usaili yenye wajumbe walioteuliwa na rais lazima ipeleke orodha fupi ya wagombea 9 kwa Rais, ambaye atatumia busara zake kuteua makamishna wasiozidi wa 5.8

Aidha, mamlaka ya kuteua mwenyekiti wa NEC na makamu mwenyekiti bado ni haki ya rais. Uwezo wa kuwaondoa wakati wowote kwa kile kinachoitwa “tabia mbaya” unatia shaka juu ya kiwango halisi cha uhuru ambacho marekebisho haya yanaleta. Ni vyema kubainisha kwamba Kifungu cha 8 (3) cha Muswada huo kinasema iwapo suala la kumwondoa Mjumbe wa Tume litatokea, Kamati ya kumshauri rais kuhusu hilo itaundwa. Hata hivyo, Rais pia ana mamlaka ya kuteua Kamati hiyo. Jambo hili linahatarisha usalama wa ajira (security of tenure) za viongozi wa NEC kwani Kamati ya kumshauri rais kuhusu hatma ya ajira zao inaweza pia kuwa ni muhuri tu wa kuidhinisha uamuzi wa Rais kumfukuza kiongozi wa NEC kwa sababu yoyote ile ambayo Rais ataona inafaa. Kwa mantiki hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Tanzania Bara, Ndg. Benson Kigaila, alisema kwa usahihi kwamba “NEC ya sasa na inayopendekezwa ni chombo cha rais cha kuratibu, kuendesha, na kusimamia uchaguzi.”9 

Hitimisho

Wakati Muswada wa NEC 2023 ukileta marekebisho fulani yanayoashiria mabadiliko kuelekea uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, unashindwa kuiondoa taasisi hiyo katika ushawishi mkubwa wa taasisi ya urais. Jambo hili linatoa fursa ya vyama vingine visivyo madarakani kutotendewa haki na NEC ambayo inaweza kushawishika kufanya kazi kwa utashi wa rais ambaye ni mwenyekiti na wakati mwingine mgombea wa urais kwa tiketi ya chama chake kilichopo madarakani. 

Kanuni ya tume huru ya uchaguzi haitumiki ili tu kudhibiti ushawishi wa chama tawala, yaani kwasasa Chama Cha Mapinduzi (CCM), bali ni kinga dhidi ya uwezekano wa chama chochote cha siasa kitakachochukua madaraka. Kanuni inahakikisha kwamba NEC inafanya kazi bila upendeleo na kwamba vitendo vyake haviyumbishwi isivyostahili na taasisi ya urais au nyingine yoyote, bila kujali rangi ya kisiasa ya serikali iliyoko madarakani. Hii bila shaka inaonyesha umuhimu wa kupatikana uhuru wa kweli, badala ya wa “mchongo”, katika utendaji kazi wa NEC nchini Tanzania.

Hivyo basi, Serikali inayoongozwa na CCM haina budi kushirikisha vyama vyote vya siasa katika mchakato huu na kuzingatia madai yao kwa umakini mkubwa kwa ajili ya uchaguzi huru na wa haki. Hapo ndipo tunaweza kusema kwa dhati kwamba mabadiliko yamefanywa ili kuboresha mchakato wa kidemokrasia nchini Tanzania. Ni lazima tuendelee kufuatilia na kutetea mageuzi ya kina kwa maandamano ya amani na njia nyinginezo zitakazopelekea uchaguzi wa kuaminika na wa haki.

***

Una maoni gani kuhusu makala hii?

Marejeo

  1. Mwananchi Digital (2024). CHADEMA yaitisha maandamano kupinga muswada sheria ya uchaguzi. Accessed on 13 January 2024. ↩︎
  2. Mwananchi (2024). RC Dar atangaza Januari 23 – 24 siku ya usafi. Accessed on 13 January 2024. ↩︎
  3. Cheeseman, N., & Elkrit, J. (2020). Understanding and Assessing Electoral Commission Independence: a New Framework. Accessed on 15 January 2024. ↩︎
  4. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977). Tume ya Uchaguzi. Accessed on 18 January 2024. ↩︎
  5. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (2015). The National Elections Act. Accessed on 18 January 2024. ↩︎
  6. Mwananchi (2023) Mahakama ya Afrika yataka mabadiliko sheria ya uchaguzi. Accessed on 18 January 2024. ↩︎
  7. Collord, M. (2021). Tanzania’s 2020 Election: Return of the One-Party State. Accessed on 15 January 2024. ↩︎
  8. Parliament of Tanzania (2023). Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Accessed on 18 January 2024. ↩︎
  9. JamiiForums (2024). Benson Kigaila: Matatizo ya Tume ya Uchaguzi Yanayojulikana hayajaguswa. Accessed on 18 January 2024. ↩︎

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *