• 9849-xxx-xxx
  • taarifa@elimuraia.com

Sakata la Mkataba wa Bandari na Utamaduni wa Kisiasa Tanzania

Muhtasari

  • Chama tawala nchini Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimejenga mazingira ya hofu na kutoaminiana ambayo yanaathiri mchakato wa kidemokrasia, hasa chini ya utawala wa hayati Rais Magufuli kuanzia mwaka 2016 hadi 2021.
  • Kukandamizwa kwa uhuru wa mikutano ya kisiasa na haki za kidemokrasia kunazuia raia kushiriki kikamilifu katika siasa, kwani huofia kushughulikiwa kwa kutoa maoni tofauti.
  • Ukosefu wa taasisi imara na utawala wa sheria chini ya utawala wa kimabavu hudhoofisha mihimili ya demokrasia, yaani uwazi na uwajibikaji.
  • Pamoja na changamoto tajwa hapo juu, uimara wa wananchi wa Tanzania na madai yao ya uwajibikaji na uwazi yanaonyesha dalili za ukomavu wa taifa kisiasa. Madai yanayoendelea ya mabadiliko ya katiba na ustawi wa utamaduni shirikishi wa kisiasa ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza jamii imara ya kidemokrasia.

Kila nchi huru duniani kote inajumuisha tamaduni moja au zaidi za kipekee za kisiasa. Tamaduni kama hizo huathiri lugha inayotumika kwa ajili ya mawasiliano, dini inayoabudiwa, na mawasiliano baina ya watu. Tamaduni hizi zimekita mizizi katika mila za jamii na uzoefu wa pamoja wa kihistoria. Pia, kila mtu ana utamaduni wa kipekee wa kisiasa kulingana na historia binafsi. Makala hii inajadili dhana ya utamaduni wa kisiasa, utafiti wake, aina zake, yaani, finyu, tawaliwa, na shirikishi, na maana zake katika mazingira ya kisiasa ya Tanzania.

Utamaduni wa Kisiasa ni nini?

Kwa mujibu wa wanasayansi ya siasa wa Marekani, Gabriel Almond na Sidney Verba (1963), utamaduni wa kisiasa unahusu mielekeo mahsusi ya kisiasa – mitazamo kuhusu mfumo wa kisiasa na taasisi zake mbalimbali na mitazamo kuhusu nafasi ya mtu binafsi katika mfumo husika. Ni zao la historia ya pamoja ya mfumo wa kisiasa na historia ya maisha ya watu binafsi katika mfumo huo. Hivyo basi, utamaduni wa kisiasa huathiriwa sio tu na matukio makubwa ya umma kama vile uchaguzi, sheria, na harakati za kijamii bali pia na uzoefu wa mtu binafsi. Mitazamo ambayo mtu anayo kuhusu masuala ya kisiasa inaweza kuathiriwa kwa kiasi kikubwa sana na uzoefu binafsi, ikiwa ni pamoja na maisha ya utotoni, malezi yake, elimu, na maadili.1

Utafiti wa Utamaduni wa Kisiasa

Utamaduni wa kisiasa wa jamii huunda maadili na mwenendo wake wa kisiasa na unapaswa kuendana na mfumo wa kisiasa unaotawala jamii husika. Kama sivyo, uhai wa mfumo wa utawala husika uko hatarini. Katika Kitabu cha II cha Republic (Jamhuri), Plato anajadili muundo wa dola-mji ufaao na elimu ya raia wake. Andiko hili linasisitiza wazo la kuandaa watu kuanzia umri mdogo kufuata kanuni na maadili ya jamii yao, ili kuhakikisha maelewano na utulivu wa jamii husika na mfumo wa kisiasa unaotawala jamii hiyo. Mchakato huu unaakisi uelewa wa sasa wa uoanishaji wa jamii na mfumo wa kisiasa (political socialization),2ambayo ni mada yetu ya siku nyingine.   

Almond na Verba (1963)

Almond & Verba (1963) walibainisha aina 3 za utamaduni wa kisiasa, yaani utamaduni wa kisiasa wenye mtazamo: 3

  • finyu,
  • tawaliwa, na
  • shirikishi

Uainishaji wa Almond na Verba wa tamaduni za kisiasa katika mpangilio finyu, tawaliwa, na shirikishi huweka msingi wa kuelewa jinsi wananchi wanavyotambua jukumu lao ndani ya mfumo wa kisiasa.

Katika utamaduni finyu wa kisiasa, raia wanakuwa na ufahamu wa kijuujuu kuhusu uwepo wa serikali kuu na wanaishi maisha yao karibia kwa kiwango cha kutosha bila kujali maamuzi yanayochukuliwa na serikali husika, na hawana taarifa za matukio ya kisiasa. Nchini Tanzania, wengi wa wananchi hawa wako katika vijiji visivyo na huduma ya mtandao au vyombo vya habari kama radio na televisheni.

Utamaduni wa kisiasa tawaliwa ni aina ambayo raia wanakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu uwepo wa serikali kuu na wanaathirika kwa kiasi kikubwa sana na maamuzi yake huku wakiwa na nafasi ndogo ya kupinga maamuzi hayo. Mtu anakuwa anafahamu siasa, wanasiasa, na taasisi za kisiasa. Hata hivyo, taasisi za kiutawala zinakuwa na ushawishi mkubwa kwa wananchi, huku maoni machache yakipokelewa kutoka kwa wananchi hao. Katika hali hii, mchakato wa ufanyaji maamuzi unatoka juu kwa watawala kwenda chini kwa watawaliwa (top – down), huku serikali ikielekeza sheria na sera ambazo lazima zifuatwe. Kwahiyo, ingawa wananchi wana ufahamu wa masuala ya kisiasa na kuelewa miundo yake, uwezo wao wa kushawishi maamuzi ya kisiasa kwa kawaida huwa na vikwazo.

Katika utamaduni wa kisiasa shirikishi, watu wanaathirika na maamuzi ya serikali, lakini na wao pia wanakuwa na uwezo wa kuathiri maamuzi ya serikali husika. Ushiriki wao huenea kwa mfumo mzima, unaojumuisha nyanja za kisiasa na kiutawala. Hii inamaanisha ushiriki wao ni pamoja na kutoa maoni (input) katika mchakato wa kisiasa na kuathiriwa na sera zinazotokana (output) na hayo maoni. Kwa mtazamo wa Almond & Verba, utamaduni wa kisiasa ni sehemu muhimu katika jamii kwani huamua jinsi wananchi wanavyoshirikiana na serikali yao na kuchagiza utendajikazi wa mfumo wa kisiasa. Hii pia inaonyesha kiwango cha imani na uhalali ambao watu wanaipa serikali yao. Aidha, wanatoa hoja kwamba utamaduni wa kisiasa shirikishi ulio thabiti ni muhimu kwa demokrasia yenye afya kwani unahimiza ushiriki hai wa wananchi katika michakato ya kufanya maamuzi na kuiwajibisha serikali.

Utamaduni wa Kisiasa Tanzania

Tanzania inaonyesha dalili za uwepo wa mchanganyiko wa tamaduni za kisiasa tawaliwa na shirikishi, hasa kwa kuzingatia watu wanaoishi maeneo ya mijini katika mikoa kama vile Dar Es Salaam, Arusha, Mbeya, na mingineyo. Licha ya kufahamu uwepo wa serikali na matendo yake, wananchi wengi mara nyingi wanahisi wana wigo mdogo wa kutokubaliana na maamuzi ya serikali, ambayo ni sifa mojawapo ya utamaduni wa kisiasa tawaliwa. Kwa kawaida, utawasikia watu hawa wenye utamaduni wa kisiasa tawaliwa wakisema maneno kama vile “Huwezi kushindana na serikali” katika mazungumzo yao ya kisiasa ya kila siku. Hata hivyo, Tanzania imekuwa na vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa, na hivyo taratibu kuelekea kwenye utamaduni wa kisiasa shirikishi. Mabadiliko haya yanadhihirika katika kuongezeka kwa mwamko wa kisiasa miongoni mwa watu, kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi katika midahalo ya kisiasa, na madai ya uwajibikaji na uwazi wa serikali.

Mabadiliko Kuelekea Utamaduni wa Kisiasa Shirikishi nchini Tanzania

Kelele za wananchi na hatua za kisheria zilizochukuliwa na Watanzania baada ya kupata taarifa ya mkataba wenye utata wa serikali ya Tanzania kuikodisha kampuni ya DP World ya Dubai kuendesha bandari ya Dar es Salaam, inaonyesha dhamira ya kipekee ya kuiwajibisha serikali yao. Shauri la kupinga uhalali wa mkataba wa bandari lililowasilishwa na wananchi wanne katika Mahakama Kuu ya Mbeya, licha ya kutupiliwa mbali haraka, linadhihirisha umakini wa wananchi na kutaka kwao kuwepo kwa uwazi katika masuala yanayohusu rasilimali za Taifa.4 Ujasiri ulioonyeshwa na watu kama Boniface Mwabukusi, Mdude Nyagali, Willibrod Slaa, na Rugemeleza Nshala katika kukosoa waziwazi “mkataba wa bandari” licha ya hatari ya kufanya hivyo ni kielelezo cha uwepo na nguvu ya Watanzania wenye utamaduni wa kisiasa shirikishi.5 

Watanzania walionyesha wasiwasi wao kwenye Mitandao ya Kijamii na majukwaa mengine kuhusu mkataba wa bandari. Bi. Maria Sarungi Tsehai, mwanaharakati maarufu nchini Tanzania, aliendesha mijadala ya mtandaoni kuhusu suala hilo kupitia jukwaa lake maarufu la “Maria Spaces” kwenye jukwaa la kidijitali la X (zamani ikiitwa Twitter). Moja ya mjadala kama huo, ulioitwa “Sakata la Bandari, Usalama na Maslahi ya Tanganyika ndani ya Muungano,” ulifanyika tarehe 8 Juni, 2023. Vilevile, majukwaa ya X ya kidijitali, kama vile “Change Tanzania” (@ChangeTanzania), yenye lengo la kutetea haki ya raia kutumia uhuru wao wa kujieleza, yanazidi kupata umaarufu na wafuasi zaidi.6

Aidha, kwa kukaidi maonyo batili ya polisi, kikundi cha vijana waliodhamiria, wakiongozwa na mwanaharakati mwenye shauku Deusdedith Soka, waliingia mtaani kuandamana Jumatatu, Juni 19, 2023. Hata hivyo, ujasiri wao huo ulidhibitiwa haraka na polisi kwa kukamatwa.7 Katika siasa za kila siku, mchanganyiko huu wa utamaduni wa kisiasa tawaliwa na shirikishi huathiri sera na utendajikazi wa serikali, hivyo kuilazimu serikali kujitahidi kuwa na uwiano kati ya kudumisha mamlaka na kutekeleza madai ya wananchi wanaozidi kuongeza ufahamu wa masuala ya kisiasa.

Isitoshe, Watanzania wanaiwajibisha serikali yao kutokana na tatizo la umeme linaloendelea nchini. Hawakubali mambo kijuujuu, bali wanadai uwazi na masuluhisho ya vitendo. Umma unasisitiza kupata maelezo ya kina kutoka kwa viongozi wa kisiasa na watendaji wakuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). Pia, Watanzania wanatoa wito wa kuwepo kwa vyanzo anuwai vya nishati na ubunifu, kama vile jua na gesi, kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika.8 Mtazamo huu wa wananchi wanaojituma kudai haki zao unaonyesha hisia kali za uwajibikaji wa kiraia katika kudai utawala bora na utoaji wa huduma za jamii.

Athari za Utawala wa Kiimla katika Utamaduni wa Kisiasa Tanzania

Kwa kubana uhuru wa kisiasa na kukandamiza upinzani, utawala wa kiimla nchini Tanzania chini ya chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), umekuza mazingira ya hofu na kutoaminiana, ambayo ni hatari kwa demokrasia yenye afya. Hili limedhihirika zaidi kuanzia mwaka 2016 hadi 2021 wakati wa utawala wa hayati Rais Magufuli pindi mikutano ya kisiasa na haki nyingine za kidemokrasia zilipopigwa marufuku au kubinywa kwa kiasi kikubwa.9 Hali hii hudhohofisha mijadala katika jamii na kuzuia ushiriki hai wa kisiasa wa raia, kwani wanaweza kuogopa kushughulikiwa kwa kutoa maoni yanayopingana na maamuzi ya serikali. Zaidi ya hayo, kutokuwepo kwa taasisi imara na utawala wa sheria chini ya utawala wa kimabavu kunadhoofisha uwazi na uwajibikaji, ambazo ni nguzo kuu za jamii ya kidemokrasia. Kwahiyo, hali kama hizo huzuia ukuaji wa utamaduni wa kisiasa shirikishi, ambapo wananchi wanahisi kuwezeshwa kushiriki katika mchakato wa kisiasa na kuwa na ushawishi katika maamuzi yatokanayo na mchakato huo.

Hitimisho

Nguvu ya taifa lolote ipo katika ushiriki wa kikamilifu wa wananchi wake katika michakato ya kiutawala na ufanyaji maamuzi. Wakati Tanzania inakabiliana na mapungufu yanayotokana na utawala wa kiimla, uimara wa raia wake, madai ya uwajibikaji, na wito wa uwazi katika usimamizi na matumizi ya rasilimali za umma ni dalili zenye kuleta matumaini. Madai ya kuwepo kwa vyanzo anuwai vya nishati na ongezeko la raia kudai utawala bora ni ushahidi wa ukuaji wa ukomavu wa kisiasa wa taifa.

Hivyo basi, ili Tanzania ipige hatua kuelekea utamaduni thabiti wa kidemokrasia, ni lazima wananchi tuendeleze harakati za mabadiliko ya katiba, tukumbatie utamaduni wa kisiasa shirikishi, na tudumishe kanuni za kidemokrasia.

Unaweza kubofya hapa kutazama video kuhusu mada iliyojadiliwa katika makala hii. Kumbuka kujiunga (subscribe) kwenye chaneli yetu ya YouTube ili kupata maudhui zaidi ya kujielimisha. Asante kwa kusoma na tunakaribisha maoni kuhusu makala hii na video yake.

***

Marejeo

  1. Almond, G., & Verba, S. (1963). The civic culture: Political attitudes and democracy in five nations. Princeton, NJ: Princeton University Press. Accessed on 20 October 2023.
    ↩︎
  2. Plato. (2008). Republic (G.R.F. Ferrari, Ed.; T. Griffith, Trans.). Cambridge University Press. Accessed on 20 October 2023. ↩︎
  3. Almond, G., & Verba, S. (1963). The civic culture: Political attitudes and democracy in five nations. Princeton, NJ: Princeton University Press.
    ↩︎
  4. The Chanzo (2023). Court Dismisses Case Against DP World Deal:”Barren of Fruits.” Accessed on 2 November 2023. 
    ↩︎
  5. Amnesty International (2023). Tanzania: Detained critics of UAE port deal must be immediately and unconditionally released. Accessed on 2 November 2023.  
    ↩︎
  6. Change Tanzania (2023). Sakata la Bandari, Usalama, na Maslahi ya Tanganyika Ndani ya Muungano. Accessed on 7 November 2023. ↩︎
  7. Mwananchi (2023). Mratibu wa maandamano kupinga uwekezaji Bandari na wenzake 10 wakamatwa. Accessed on 6 November 2023. 
    ↩︎
  8. Voice of America (2023). Watanzania waitaka TANESCO kutoa taarifa rasmi kuhusu mgao wa umeme. Accessed on 6 November 2023. ↩︎
  9. Amnesty International (2020). Tanzania: Laws weaponized to undermine political and civil freedoms ahead of elections. Accessed on 6 November 2023. 
    ↩︎

2 thoughts on “Sakata la Mkataba wa Bandari na Utamaduni wa Kisiasa Tanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *